Business
KPA yatoa ilani ya siku 14 kwa kampuni za meli
Mamlaka ya bandari nchini KPA imeanzisha zoezi la kusafisha maeneo ya kuhifadhi mizigo katika bandari ya Mombasa katika juhudi za kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha usalama na ufanisi wa shughuli za bandari,.
Taarifa rasmi ya KPA ilisema kuwa, baada ya ukaguzi wa kina baadhi ya makasha na mizigo bado yanasalia bandarini licha ya kuamuliwa kuwa yamekataliwa kwa mujibu wa sheria na hivyo yanapaswa kuondolewa au kuharibiwa.
KPA sasa inazipa kampuni za meli muda wa siku 14 kuhakikisha zinashughulikia uondoaji au uharibifu wa mizigo hiyo.
Mamlaka hiyo ilisisitiza kuwa endapo muda huo utapita bila hatua kuchukuliwa, bandari italazimika kuharibu au kuondoa mizigo hiyo kwa gharama ya kampuni husika, bila kuwahusisha tena wamiliki wa mizigo hiyo.
Hatua hii inalenga kuongeza nafasi bandarini na kuhakikisha huduma bora kwa wateja wanaotegemea bandari ya Mombasa kusafirisha na kupokea bidhaa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.