News
KPA yaekeza mashine za kufyonza vumbi bandarini Mombasa.
Mamlaka ya bandari nchini KPA imeanza kutumia mashine za kufyonza ukungu maarufu mist blower fogging units katika bandari ya Mombasa, ili kudhibiti vumbi hatari linalotokana na shughuli za upakuaji mizigo kwa wingi kama vile klinka, makaa ya mawe na jipsam.
Mradi huu wa majaribio ni sehemu ya sera ya “Bandari Kijani”, inayolenga kulinda afya ya wafanyakazi bandarini, watumiaji, pamoja na wakaazi wa maeneo jirani.
Mashine hizo zimewekwa katika gati namba 9 na 10, na zinatarajiwa kufanya kazi kwa pamoja na vifaa vingine vinavyolinda mazingira kama vile eco-hoppers, ili kupunguza kuenea kwa chembechembe ndogo za vumbi hewani.
Meneja mkuu wa maendeleo ya miundombinu katika KPA, Mhandisi Mathews Amuti, alisema hatua hii ni sehemu ya juhudi za KPA kuzingatia viwango vya kimataifa katika utunzaji wa mazingira na uendeshaji wa shughuli zake.
Amuti alisema kuwa utendaji wa mashine hizo utafanyiwa tathmini kabla ya kuamua kama teknolojia hiyo itaenezwa katika maeneo mengine ya bandari.
Aidha mhandisi huyo aliongeza kuwa mradi huu ni moja wapo ya juhudi za kuimarisha uendelevu wa shughuli za bandari na kupunguza athari zake kwa mazingira na jamii.
Taarifa ya Mwanahabari wetu