Sports

Kocha wa Uingereza Thomas Tuchel akataa madai ya “laana” huku akilenga kuvunja ukame wa miaka 60 wa mataji makubwa

Published

on

Kocha mkuu wa Uingereza, Thomas Tuchel, amesisitiza kwamba hakuna “laana” inayoisumbua timu yake anapoangazia kukatiza ukame wa karibu miaka 60 bila kushinda taji kubwa la kimataifa.

Mara ya pekee Uingereza kushinda taji kubwa ilikuwa mwaka 1966 walipoandaa Kombe la Dunia na kuifunga Ujerumani Magharibi kwenye fainali.

Timu hiyo ilikaribia mara kadhaa kuvunja ukame huo chini ya kocha wa zamani Gareth Southgate, ikipoteza fainali mbili mfululizo za Euro, pamoja na kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 na robo fainali mwaka 2022.

Wakati huo huo, timu ya wanawake ya Uingereza imepata mafanikio chini ya Sarina Wiegman, ikishinda mataji mawili mfululizo ya Euro mwaka 2022 na 2025. Timu ya wanaume ya chini ya miaka 21 pia ni mabingwa wa Ulaya mara mbili, baada ya kutetea taji lao la 2023 kwa ushindi nchini Slovakia mwezi Juni.

“Hapana kabisa,” Tuchel alisema alipoulizwa kama anahisi shinikizo zaidi kutokana na mafanikio ya timu ya wanawake na vijana.

“Kama kuna lolote, basi ni ishara nzuri na nilifurahi sana kwa Sarina na (kocha wa U21) Lee (Carsley) kwa sababu waliweza kufanikisha na wakatoa juhudi kubwa, mafanikio makubwa kwa kushinda mataji mfululizo…

“Inawezekana kushinda taji na Uingereza, hakuna laana kwa timu za Kiingereza na ni ishara nzuri. Tutafanya kila tuwezalo kufuata mfano wao.”

Uingereza itakabiliana na Andorra siku ya Jumamosi katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Mexico na Kanada, kisha kuvaana na Serbia mjini Belgrade siku ya Jumanne.

“Ninapata ushauri mwingi, hilo ni hakika, lakini mara zote kwa njia ya kirafiki,” Tuchel, aliyewahi kuwa kocha wa Chelsea, alisema kuhusu mashabiki wa Uingereza.
“Wengi wao huniambia tu, ‘Leta nyumbani, Thomas’. Hiyo ndiyo kazi haswa.”

Beki wa Manchester City, John Stones, ameondoka kwenye kikosi kutokana na jeraha na hatashiriki michezo ijayo.

Stones hajachezea taifa lake tangu Oktoba mwaka jana na amebakia na jumla ya mechi 83 za kimataifa.

Latvia na Albania ndizo timu zingine katika Kundi K la kufuzu Ulaya, ambapo mshindi wa kundi atajipatia nafasi ya moja kwa moja kwenye Kombe la Dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version