News
Kenya yaadhimisha miaka 15 ya Katiba
Kenya inaadhimisha miaka 15 ya Katiba mpya tangu kubuniwa rasmi mwaka wa 2010 chini ya utawala wa Hayati Mwai Kibaki kufuatia shinikizo la miaka mingi ya mifumo ya majimbo yaliyoanzishwa na Marehemu Ronald Ngala wakati wa utawala wa Hayati Mzee Jomo Kanyatta.
Shinikizo hizo hazikuishia wakati huo licha ya kuzongwa na siasa za kibepare, Mwanasiasa Raila Odinga wakati huo alianzisha vuguvugu la vyama vingi na kuchangia kuyumbishwa kwa mpango huo na kupelekea utawala wa Rais wa pili wa Kenya Hayati Daniel Arap Moi kuruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka wa 1992.
Kutokana na kwamba wakenya walikuwa na nia ya kushuhudia mabadiliko nchini na uhuru wa kujieleza, walianzisha kura ya maoni yani ‘Referendum’ na kuafikia kubuniwa kwa katiba mpya mwaka wa 2010.
Kubuniwa kwa Katiba hiyo mpya kulichangia mabadiliko mengi nchini ya kiuongozi, kielimu, huru wa kujieleza, kuandamana na demokrasia ya taifa kote nchini.
Mnamo Agosti 25, 2025 Rais William Ruto alitangaza kwamba Agosti 27, itakuwa siku ya kitaifa ya Katiba Dei ambayo itakuwa ikiadhimishwa kila mwaka.
Tangazo hilo la rais lilifafanua zaidi kwamba siku hiyo itakuwa siku ya kawaida ya kazi na wala sio siku ya kitaifa ya mapumziko na kwamba itawawezesha wakenya kufahamu masuala mbalimbali ya Katiba, utawala wa sheria na mazungumzo ya kitaifa.

Rais William Ruto akitia saini sheria mpya kuhusu Katiba Dei kama siku ya kitaifa
Aidha lengo kuu la Katiba Dei ni kuangazia safari ya kidemokrasia ya Kenya na kuhimiza haki ya umma katika mijadala mbalimbali ya utawala kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kote nchini.
Hata hivyo himizo zaidi ni kwa mihimili tatu ya serikali, ngazi zote mbili za kiutawala na taasisi za kielimu zitahitajika kuandaa na kushiriki katika shughuli za umma ili kukuza uelewa wa Katiba na ushirikishwaji wa umma.
Baadhi ya wakenya walisema licha ya Katiba ya Kenya kutimiza miaka 15 tangu kubuniwa rasmi, viongozi wengi wanaonekana kutozingatia muongozo wa Katiba hiyo sawa na kanuni zake huku wakisema kwamba ni muhimu kwa kila mmoja wakiwemo viongozi kuwajibika na kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao kwa mujibu wa kanuni na sheria za Katiba.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi