News

Kenya, Ufaransa kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Published

on

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitiza ushirikiano kati ya ufaransa na Kenya katika kutetea ajenda ya kimataifa inayojumuisha maendeleo endelevu na hatua za kukabili mabadiliko ya tabia nchi, kabla ya mkutano mwengine utakaohusisha bara afrika na Ufaransa jijini Nairobi mwaka ujao.

Akizungumza kutoka Seville katika kongamano la ngazi ya juu kuhusu ushirikiano wa kimataifa, Rais Macron alisisitiza maono yake ya pamoja na Rais William Ruto akisema hakuna nchi inapaswa kulazimishwa kuchagua kati ya maendeleo ya kiuchumi na ulinzi wa mazingira.

“Pamoja na Rais William Ruto, tunashiriki ahadi moja: kwamba hakuna nchi inapaswa kuchagua kati ya maendeleo na kulinda sayari,” Macron alisema. “Haya ndiyo matamanio tunayoleta leo Seville na washirika wetu, kama sehemu ya mkataba wa mafanikio, watu na sayari uliozinduliwa miaka miwili iliyopita huko Paris.”

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kuendeleza ajenda hii katika kongamano la Afrika na Ufaransa 2026, ambalo litasimamiwa na Kenya na Ufaransa jijini Nairobi.

Mkutano huo unatazamiwa kuangazia ushirikiano wa kibunifu unaoshughulikia malengo ya maendeleo endelevu ya afrika sambamba na kukuza ukuaji wa uchumi jumuishi.

Rais Macron pia alisema kuwa Kenya na Ufaransa zinashirikiana kikamilifu katika miradi muhimu ya nchi mbili kama vile mpito wa nishati, miundombinu endelevu ya uchukuzi na maendeleo ya kilimo.

Alisema miradi hii, inaonyesha aina ya ushirikiano wa kimantiki unaohitajika ili kufikia maendeleo yanayostahimili hali ya hewa.

Mbali na ushirikiano wa kiuchumi na kimazingira, marais hao wawili walisisitiza dhamira yao ya pamoja ya kukuza amani na usalama kote barani Afrika, hasa katika eneo la Maziwa Makuu, Sudan na Somalia.

“Tulisisitiza dhamira yetu ya pamoja ya amani na usalama katika eneo la Maziwa Makuu, Sudan, na Somalia,” Rais Macron alibainisha, akisisitiza jukumu la Ufaransa na Kenya kusaidia utulivu wa kikanda kupitia ushirikiano wa kidiplomasia na usaidizi wa maendeleo.

Tarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version