Entertainment
#Janjaruka254: Safari ya Omwami ya Kuchekesha Dunia
Kicheko ni dawa, lakini safari ya kumfanya mtu acheke si ya mchezo. Hii ni kauli inayomwelezea vyema Omwami Comedian, mchekeshaji anayezidi kung’aa kwenye anga la burudani humu nchini. Katika mahojiano ya kipekee na Janjaruka 254, Omwami amefunguka kuhusu safari yake ya kuwa mchekeshaji, akieleza changamoto, matumaini, na nguvu ya kutokata tamaa.
Omwami anasema kipaji chake cha ucheshi kilianza kujionyesha tangu akiwa mtoto. Alikuwa na tabia ya kunakili sauti na maneno ya wageni waliotembelea familia yao, kisha baadaye kuwaigiza mara tu walipoondoka. “Nilikuwa kama runinga ya familia. Watu walinifurahia lakini pia walikuwa makini wakija kwetu, maana walijua nitaigiza kila kitu walichosema,” Omwami alisema kwa tabasamu.
Akiwa shule ya upili, Omwami alijiunga na kundi la waigizaji. Hapo ndipo kipaji chake kilianza kung’aa rasmi. Hata hivyo, safari hiyo haikuwa rahisi kwani mama yake hakufurahishwa na ushiriki wake katika sanaa akiamini angerudi nyuma masomoni.
“Mama alikuja shule kuniambia niachane na drama club, lakini mwalimu mkuu alikataa kwa sababu aliona nina kipaji,” alisema.
Omwami anasema kupata nafasi ya kuigiza kwenye kipindi maarufu cha Churchill Show haikuwa lelemama. Alifanya auditions zaidi ya tatu kabla ya kupata nafasi ya kuonesha uwezo wake.
“Ilichukua muda na maombi. Lakini siku moja nilipofanikisha, nilijua ndoto yangu inaanza kutimia,” alisema.
Katika harakati zake, Omwami hakusahau kumtaja mchekeshaji maarufu Eric Omondi na Victor Ber kama watu waliompa moyo wa kuendelea kufanya anachokipenda. “Eric aliniambia nina uwezo mkubwa na nisikate tamaa. Hilo lilinipa nguvu kuendelea na leo hii, naona matunda ya uvumilivu,” alieleza kwa shukrani.
Omwami anahitimisha kwa kutoa wosia kwa vijana na mtu yeyote anayefuatilia ndoto yake. “Usikate tamaa. Haijalishi changamoto ni kubwa kiasi gani, ukijitahidi na kuomba, siku moja utafanikiwa.”
Safari ya Omwami ni ushuhuda kuwa mafanikio hayaji kwa urahisi. Inahitaji bidii, kujitoa, na imani. Kwa wale wanaotafuta nafasi yao kwenye sanaa au nyanja nyingine yoyote, hadithi ya Omwami ni mfano wa kuigwa – kuwa huwezi chekesha dunia kabla hujajifunza kuvumilia vizingiti vyake.