News

Hatma ya Gavana Mutai kuwekwa wazi na bunge la Seneti

Published

on

Kesi inayosubiriwa kwa hamu ya kumuondoa madarakani Gavana wa Kericho Erick Mutai, imeanza rasmi katika bunge la Seneti.

Kulingana na ratiba rasmi iliyotolewa na Karani wa bunge la Seneti, kikao kilitarajiwa kuanza saa tatu asubuhi kwa mkutano wa faraghani wa maandalizi ya maseneta.

Kikao hiki cha ndani kililenga kuwapa wanachama nafasi ya kupitia kanuni za mashauri na mwelekeo wa kesi kabla ya ufunguzi rasmi.

Kikao cha hadhara kilitarajiwa kuanza saa nne asubuhi kwa taratibu za awali, ikiwemo kusomwa kwa wajibu wa Seneti na utambulisho wa pande zote mbili.

Wajumbe wa Bunge la kaunti ya Kericho waliowasilisha mashtaka hayo walitambulishwa rasmi pamoja na mawakili wao.

Gavana Mutai na timu yake ya utetezi pia walitarajiwa kuwasilishwa mbele ya Baraza.

Saa tano asubuhi, mashtaka dhidi ya gavana yalisomwa, yakitoa mwelekeo wa mijadala ya siku.

Baada ya hapo kulifanyika kikao cha dakika 90 cha kushughulikia maswali na hoja za awali kabla ya kuanza kwa usikilizaji wa ushahidi.

Baada ya mapumziko ya chakula cha mchana kuanzia saa saba mchana hadi saa nane na nusu alasiri, pande zote zilipewa muda wa kutoa kauli za ufunguzi.

Bunge la kaunti, kupitia wawakilishi wake lilipewa dakika 30 kueleza hoja zake kisha timu ya utetezi ya Gavana Mutai pia iliwekewa muda wa dakika 30 kujibu.

Sehemu kubwa ya kikao cha alasiri, kuanzia saa tisa na nusu hadi saa kumi na mbili na nusu jioni, ililenga uwasilishaji wa ushahidi.

Bunge la kaunti lilitengewa muda wa saa tatu kuwasilisha mashahidi wake na kufanya upekuzi wa mahojiano.

Upande wa gavana ulipewa muda wa saa mbili kuuliza maswali ya majibu kwa mashahidi hao.

Kesi ya Gavana Mutai imevutia hisia kote nchini, si Kericho pekee, kwani itajaribu nguvu za kisiasa kati ya mabunge ya kaunti na magavana, huku ikisisitiza jukumu la kikatiba la Seneti kama msuluhishi wa migogoro ya kuondoa viongozi madarakani.

Bunge la kaunti ya Kericho limewakilishwa na mawakili 12 wakiongozwa na Elisha Ongoya. Wanaosaidia ni Kimutai Bosek, Sharon Mibey, Elias Mutuma, Hillary Kiplangat, Brian Langat, Geoffrey Langat na Victor Kibet.

Wengine ni Evans Kiplangat, Elvis Kipkorir, Joel Wakhungu na Vincent Kipronoh.

Orodha iliyowasilishwa Seneti inajumuisha maafisa wanne wa kisheria, akiwemo Brian Maingi, Ian Kiplangat, Mitchel Mutuma na Japhet Koech.

Mutai, kwa upande wake, anawakilishwa na mawakili sita wakiongozwa na Katwa Kigen, Peter Wanyama, Rose Thiong’o, Doris Ng’eno, Joash Mitei na Evanson Kirui.

Wakati wa kutoa hotuba ya utangulizi, Wakili mkuu wa Bunge la kaunti, Elisha Ongoya, aliomba kuruhusiwa kuwasilisha ushahidi mpya, jambo lililopingwa vikali na timu ya utetezi ya Mutai.

“Mheshimiwa Spika, tunapinga vikali jaribio la kuwasilisha ushahidi mpya kwa wakati huu kwa sababu hatutakuwa na nafasi ya kuupitia na kujibu kwa kuzingatia kuwa leo tumepangiwa usikilizaji wa kesi,” alisema Kigen.

Nyaraka hizo zilijumuisha vocha za malipo za idara ya kilimo, ardhi na mipango ya miji ambazo hazikuwa zimewasilishwa awali.

Pia zilikuwa na taarifa za mashahidi, barua za uhamisho wa wafanyakazi, taarifa za M-Pesa, ripoti ya kamati ya ADHOC ya kazi mtaani, rekodi za malipo na barua za kufutwa kazi miongoni mwa nyingine.

Hata hivyo, katika uamuzi wake Spika Amason Kingi aliruhusu nyaraka hizo kuwasilishwa.

“Niliposikia maelezo ya wakili wa bunge la kaunti, alibainisha kwamba nyaraka hizo ziliachwa kwa bahati mbaya wakati wa kuandaa, hazileti ushahidi mpya… kwa hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 30 ya taratibu za kesi, nitaruhusu nyaraka hizo kuwasilishwa,” alisema Kingi.

Taarifa ya Elizabeth Mwende

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version