News

Biwot: Familia zilizoathirika na ujenzi wa barabara ya Kilifi-Mtwapa zafidiwa

Published

on

Idara ya usalama kaunti ya Kilifi imesema serikali inaendelea na zoezi la kufidia familia zilizoathirika na ujenzi wa barabara kuu ya Kilifi kuelekea Mtwapa.

Kamisha wa kaunti ya Kilifi Josephat Biwot alidokeza kuwa kwa sasa maafisa wa shirika la Kenya power wanaendelea kuondoa nyaya za stima ili kutoa nafasi kwa mkandarasi kuendelea na shughuli za ujenzi.

Vile vile Biwot alisema ujenzi daraja mbili kubwa kaunti ya Kilifi unaendelea pamoja na ujenzi wa barabara ya Sabaki Sosoni kueleke Baricho hadi Baolala.

“Ujenzi wa barabara kuu ya Kilifi kuelekea Mtwapa unaendelea vyema, tunachokifanya sasa ni kufidia walioathirika, pia kenya power inaondoa nyaya kupisha mwanakandarasi kuendelea na ujenzi, vile vile ujenzi wa daraja mbili kuu kilifi unaendelea hasa ya Galana Kulalu na Baricho”, alisema Biwot.

Vile vile Kamishna huyo alidokeza kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali inayoambatanishwa na sekta ya uchumi wa bahari.

“Upande wa uchumi wa bahari miradi mingi inaendelea mfano ujenzi wa eneo la kuegesha boti kilifi, pia tunajenga makao makuu ya eneo la samaki ya kaunti, tuko na soko la samaki Malindi, tuko na eneo la kuhifadhi samaki la kichwa cha kati ambalo limekamilika na liligharimu shilingi milioni 250”, aliongeza Biwot.

Wakati huo huo wadau wa sekta ya Uvuvi eneo la Ngomeni wakiongozwa na Mwenyekiti wa Ngomeni BMU Said Athman aliitaka serikali kufuatilia kwa kina fedha zinazotolewa na serikali kudaidi miradi ya wavuvi.

“Tunapewa pesa ya makundi kwa mfano shilingi milioni tatu, ile pesa mpaka ikifikia jamii imeliwa, kwa mfano unapewa boti lakini halina vifaa sababu ile pesa imeliwa juu na maofisa mpaka ikifika nyanjani imeisha”, alisema Athman.

Mwenyekiti wa Ngomeni BMU Said Athman akizungumza na wanahabari Kilifi.

Taarifa ya Joseph Jira.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version