News

Familia ya Kenyatta yatoa milioni 1.5 kusaidia Kanisa Katoliki Watamu

Published

on

Familia ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta imetoa shilingi milioni 1.5 kusaidia ujenzi wa kituo cha uchungaji cha Stella Maris Pastoral Center katika eneo la Watamu katika kaunti ya Kilifi.

Rais mstaafu Kenyatta alikuwa ameandamana na mkewe Bi Margaret Kenyatta pamoja na familia yao akiwemo Maina Gakuo na mkewe Anna Kadzo Gakuo Kenyatta, walipokelewa na Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Malindi Willybard Lagho.

Kenyatta alilipongeza jimbo Katoliki la Malindi kwa kujitolea kujiimarisha kifedha kupitia mradi huo na kwamba aliahidi kulisaidia jimbo hilo hadi kituo hicho cha kichungaji kitakapokamilika.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Bi Margaret Kenyatta, Askofu wa Malindi Willybard Lagho pamoja na mapadre na familia ya Kenyatta katika kituo cha Stella Maris, Watamu {picha kwa hisani}

Naye Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Malindi Willybard Lagho, alishukuru msaada huo kutoka kwa familia ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa niaba ya Jumuiya ya Kikatoliki huku akipongeza juhudi za Mapadre wa jimbo hilo la Malindi katika kufanikisha uendelezi wa ujenzi wa kituo hicho hasa Padre Bernard Malasi, Padre Stephen Kadenge na Padre David Ndwiga.

Askofu Lagho, hata hivyo aliishukuru familia ya Kenyatta kwa ukarimu wao na kuwahakikishia kwamba dayosisi ya Malindi itawapa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha kichungaji.

Kituo hicho cha kichungaji cha Stella Maris kinatarajiwa kutumika kama kitovu cha kiroho, kijamii na kiuchumi kwa jumuiya ya kikatoliki na Jimbo kuu la Malindi mara kitakapokamilika.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version