Muungano wa mawakala wa usafiri wa baharini nchini (KSAA), umeibua wasiwasi kuhusu ongezeko la gharama za uendeshaji wa shughuli za usafiri wa baharini katika bandari ya Mombasa.
Muungano huo pia ulitahadharisha kwamba ucheleweshaji na ukosefu wa ufanisi, unahatarisha ushindani wa bandari hiyo ambayo ni kitovu kikuu cha biashara nchini.
Akizungumza na Wanahabari Afisa mkuu mtendaji wa Muungano huo Elijah Mbaru, alisema sekta ya usafiri wa baharini ilikumbwa na mabadiliko makubwa mwaka uliopita, hali iliyosababisha hasara kwa kampuni za usafirishaji.
Mbaru alisema meli nyingi zinatumia muda mwingi kusubiri vibali na nafasi ya kudokoa, jambo ambalo limeongeza gharama za mafuta, ada za kuchelewa na gharama nyingine za uendeshaji katika bandari ya Mombasa.
Wakati huo huo Muungano huo uliitaka serikali na wadau husika kuboresha ufanisi, kupunguza ucheleweshaji, na kuongeza miundo mbinu ili kuhakikisha bandari ya Mombasa inaendelea kuimarika kimataifa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
