Kaunti ya Kilifi yawaagiza wauguzi kusitisha mgomo na kurejea kazini

Kaunti ya Kilifi yawaagiza wauguzi kusitisha mgomo na kurejea kazini

Huku mgomo wa wauguzi wa kaunti ya Kilifi ukiingia siku yake ya pili, na kusambaratisha utaoji wa huduma za afya, Serikali ya kaunti hiyo imejitokeza na kuzungumzia suala hilo.

Kati ya lalama zilizochangia Wauguzi kushiriki mgomo ni pamoja na malimbikizi ya mishahara ya mwezi Januari na Februari mwaka wa 2021, kutopandishwa vyeo, mazingira duni ya kazi miongoni mwa masuala mengine.

Msemaji wa serikali ya kaunti ya Kilifi Jonathan Mativo alisema japo serikali ya kaunti hiyo inafahamu kuhusu malimbikizi hayo ya mishahara ikiwemo malimbikizi ya deni la zaidi ya shilingi bilioni 11, kamati maalum imebuniwa kusawazisha suala hilo.

“Tunajua kuna malimbikizi ya deni la zaidi ya shilingi bilioni 11 lakini hiyo haihusiani na masuala haya ya mgomo wa wauguzi, ndiposa tunasema kuna jopo liliundwa kuangalia suala hilo la baada ya siku 45 litatoa ripoti yake”, alisema Mativo

Mativo, aliwarai wauguzi hao kurejea kazini na kushiriki mazungumzo ya kutatua matakwa yao ili kuhakikisha huduma za afya katika hospitali na zahanati za umma, hazikumbwi na changamoto.

“Tuna waagiza wauguzi wote walio katika mgomo kurejea kazini mara moja na kushiriki mazungumzo ya kutatua matakwa yao, tunajua kwamba kuna malimbikizi ya mishahara yao ya mwezi Januari na Februari mwaka wa 2021 lakini hiyo hatuaezilipa kwa sababu kuna kesi Mahakamani na Jaji Mbaru alitoa uamuzi wa wazi kabisa kuhusu suala hilo,” alisema Mativo.

Waziri wa Afya katika serikali ya kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo alitoa onyo kali kwa Muungano wa wauguzi hao kwamba utachukuliwa hatua za kinidhimu iwapo utawashurutisha wauguzi watakaorejea kazini ama kukatiza huduma kwenye hospitali za kaunti.

“Taratibu za kupandisha wauguzi vyuo ziko na tunawaambia wauguzi warudi kazini na wale ambao wanaendelea na kazi hatutarusu watishie ama mtu kutatiza shughuli za hospitali, wale watapatikana tutawachukulia hatua na hata kuwafungulia mashtaka Mahakamani”, alifafanua Mwarogo.

Akizungumzia mgomo huo wa wauguzi, Mwenyekiti wa bodi ya huduma za umma kaunti ya Kilifi Albert Muturi alisema licha ya kufanya vikao kadhaa na Muungano wa wauguzi, na hata wauguzi 530 kupandishwa vyeo, hawafai kugoma.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi