KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa

KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa

Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.

Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.

Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.

Taarifa ya Mwanahabari wetu