Gharama ya matibabu na uhaba wa dawa umeathiri juhudi za kudhibiti ugonjwa wa figo

Gharama ya matibabu na uhaba wa dawa umeathiri juhudi za kudhibiti ugonjwa wa figo

Ulimwengu umeadhimisha siku ya kimatiafa ya Figo dunianihuku ikibainika kuwa gharama kubwa za matibabu pamoja na uhaba wa dawa katika hospitali za umma nchini ni miongoni mwa changamoto kuu zinazokwamisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa figo.

Wagonjwa wa figo waliopata matibabu na wanaoendelea kutumia dawa walisema hali hiyo imefanya matibabu kuwa mzigo mkubwa kwao na familia zao.

Wakizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Figo duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi, kaunti ya Kilifi, wagonjwa hao waliitaka serikali kuingilia kati ili kupunguza gharama za matibabu na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa urahisi katika hospitali za umma.

Aidha, wagonjwa hao walilalamikia ukosefu wa taasisi za kupandikiza figo nchini wakisema hali hiyo inalazimu baadhi yao kusafiri hadi mataifa ya nje ili kupata huduma hiyo, jambo linaloongeza gharama na kuchelewesha matibabu.

Kwa upande wao, wauguzi wa ugonjwa wa figo wakiongozwa na Daniel Masha pamoja na Fatuma Bashir walikiri kuwepo kwa changamoto hizo huku wakisema kuna haja ya serikali kubuni mikakati madhubuti ya kuhakikisha gharama za matibabu ya figo zinadhibitiwa kikamilifu kupitia mpango wa Bima ya Afya ya Jamii (SHA).

Masha pia alipendekeza kuanzishwa kwa taasisi maalum za kupandikiza figo katika kila kaunti, pamoja na kuajiri wataalamu wa kutosha ili kuboresha huduma kwa wagonjwa wa figo nchini.

Naye mtaalamu wa afya ya figo, Daktari Andrew, alisisitiza umuhimu wa kuongeza hamasa kwa umma kuhusu ugonjwa wa figo. Amesema uhamasishaji utasaidia wananchi kutambua dalili mapema na kuchukua hatua za matibabu kwa wakati.

Daktari Andrew pia aliwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufanyiwa uchunguzi wa afya mara kwa mara, akipendekeza kila mtu kutembelea kituo cha afya angalau mara moja kwa mwaka kwa ajili ya uchunguzi wa jumla wa afya.

Maadhimisho ya siku ya Figo duniani hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu magonjwa ya figo, umuhimu wa kinga, na upatikanaji wa matibabu kwa wagonjwa duniani kote.

Taarifa ya Elizabeth Mwende