Serikali imesema imechukua hatua za dharura ili kuongeza ufanisi katika bandari ya Mombasa, kufuatia ongezeko kubwa la mizigo linalosababisha msongamano mkubwa wa meli bandarini humo.
Ongezeko hilo limehusishwa na uchaguzi mkuu uliokamilika hivi majuzi nchini Tanzania, ambao umechochea kuongezeka kwa shehena za bidhaa zinazoingizwa nchini, hali inayosababisha zaidi ya meli 22 kusubiri kushushwa mizigo.
Mkurugenzi mkuu wa KPA nahodha William Ruto alisema kwa kawaida bandari ya Mombasa hushughulikia takriban konteina 3,520 kwa siku, lakini wingi wa mizigo ulioshuhudiwa umepelekea uwezo wake kufikia kiwango cha juu zidi.
Aidha, Ruto alidokeza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, halmashauri ya bandari nchini (KPA) kwa ushirikiano na mamlaka ya mapato nchini (KRA) zimeweka kanuni mpya zinazolenga kupunguza msongamano na kuongeza kasi ya upakuaji mizigo.
Ruto alielekeza kuwa, waagizaji wa mizigo ya ndani watalazimika kushughulikia mizigo yao kupitia vituo vya (CFS) mjini Mombasa, huku mizigo ya usafirishaji wa nchi jirani, ikitakiwa kushuhulikiwa katika vituo vya mizigo vya ndani vya Nairobi au Naivasha (ICD).
Aidha, KPA ilizitaka meli zinazobeba mizigo ya kusafirishwa kuelekeza safari zao katika Bandari ya Lamu ili kupunguza msongamano katika bandari ya Mombasa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
