Wadau wa sekta ya utalii walalamikia uhaba wa maji Kilifi

Wadau wa sekta ya utalii walalamikia uhaba wa maji Kilifi

Wadau katika sekta ya utalii eneo la Watamu kaunti ya Kilifi wanasema uhaba wa maji ambao unashuhudiwa kwa mda mrefu unaathiri biashara zao.

Kulingana na wadau hao, walitishia kufunga zaidi ya hoteli 75 kutokana na uhaba wa maji ambao umeshuhudiwa kwa miezi miwili sasa.

Aidha walisema kuwa kwa sasa watalii wengi wameanza kuhamia maeneo jirani ya Zanzibar hali ambayo inaathiri uchumi wa eneo hilo.

Waliitaka idara husika kuingilia kati na kuhakikisha tatizo la maji linatatuliwa ili kuwawezesha kuendeleza shuhuli zao huku wakionya kuwa hatua hiyo huenda ikaathiri wafanyikazi wapatao elfu 10 ambao wanategemea sekta ya utalii hali itakayoathiri uchumi wa kaunti ya Kilifi.

“Tayari zaidi ya wawekezaji 30 wamesema kuwa mawakala wao wa kimataifa wametishia kusitisha mkataba na kuelekeza huduma zao kwenye maeneo mbadala yenye huduma thabiti hali ambayo itapelekea hali ya kiuchumi kwa wanaotegemea utalii kuwa mbaya zaidi.” Walisema wadau hao wa utalii.

Taarifa ya Pauline Mwango