Wadau wa sekta ya utalii eneo la Pwani wametoa wito kwa serikali kufungua anga ya Kenya kwa mashirika zaidi ya ndege za kimataifa, wakisema kuwa hatua hiyo itapunguza gharama za usafiri na kuongeza idadi ya watalii.
Wakizungumza jijini Mombasa, wadau hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha utalii wa biashara na mikutano wakisema eneo la Pwani ni kivutio kikubwa cha wageni wa kimataifa.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka uliopita, kati ya mikutano ya vyama zaidi ya 11,000 iliyofanyika duniani kote, Kenya iliandaa mikutano 29 pekee, ambapo mikutano mitano tu ilifanyika Pwani.
Hii inaashiria kuwa miakakati zaidi inastahili kuwekwa ili kuhakikisha kuwa mikutano zaidi ya kibiashara inafanyika eneo la pwani hali ambayo itainua uchumi wa eneo hili.
“Serikali kuu kwa ushirikiano na serikali za kaunti zinastahili kuimarisha utalii biashara kwa kufungua anga zaidi jambo ambalo litaimarisha uchumi.”
Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir alisema kuwa kaunti hiyo ina uwezo wa kupokea hadi wageni 3,000 kwa siku kupitia usafiri wa ndege, sawa na wageni milioni 1.95 kwa mwaka.
Kwa sasa, Kenya inashikilia nafasi ya 63 duniani katika utalii wa mikutano, hali inayoonyesha haja ya maboresho makubwa katika sekta hiyo.
“ Kaunti ya Mombasa iko na uwezo mkubwa wa kupokea wageni wa nje na wandani ambao ni zaidi milioni 1.95 na kwa sasa tunaweka mikakati zaidi kuboresha utalii ili kubuni nafasi za ajira kwa vijana wetu.
Taarifa ya Pauline Mwango