Rebecca Miano:Sekta ya utalii nchini kuimarika zaidi

Rebecca Miano:Sekta ya utalii nchini kuimarika zaidi

Waziri wa Utalii, Rebecca Miano, amesema Kenya inalenga kupokea watalii milioni 5 wa kimataifa na wengine takriban milioni 10 wa ndani kwa ndani.

Akizungumza jijini Mombasa katika kongamano la kuadhimisha siku ya kimataifa ya utalii nchini, waziri Miano alisema serikali pia inalenga kufungua anga huru ili kuruhusu watalii wengi wakimataifa kuzuru Kenya.

Wakati huo huo, waziri Miano aliwataka viongozi wa serikali za kaunti kukumbatia tamaduni na masuala ya uvumbuzi na ubunifu kama vyanzo vikuu vya kuvutia watalii.

Katika hafla hiyo vile vile, Miano alisema chuo cha utalii cha Ronald Ngala, mradi unaopatikana katika eneo la Vipingo kaunti ya Kilifi na ulioanza kujengwa tangu mwaka 2010, utakamilika hivi karibuni ili kuanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaonuia kusomea taaluma mbalimbali za utalii.

Waziri Miano alidokeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa chuo hicho kutaimairisha sekta ya utalii kwa kuogeza idadi ya wataalamu wa ndani na hivyo kuboresha huduma kwa watalii nchini.

Kauli yake imeugwa mkono na katibu mkuu katika idara ya utalii John Ololtuaa akisema kwamba serikali imejitolea kuhakikisha sekta ya utalii imeimarika.

Naye gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir alisisitiza ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti ili kuboresha sera za utalii ili kuwavutia watalii zaidi kutoka ughaibuni.

Tarifa ya Mwanahabari wetu