Viongozi wa Chama tawala cha UDA kaunti ya Kilifi wamekutana kuangazia mipango na mikakati ya kuimarisha chama hicho mashinani.
Kati ya masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na viongozi hao kufanya kazi pamoja na jamii katika ngazi ya mashinani ili kuendeleza maendeleo, uongozi jumuishi na dhamira ya kujenga mustakabali imara kwa mwananchi.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Naibu Kiongozi wa wengi bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya, viongozi hao waliangazia pia suala la kuendeleza malengo ya chama cha UDA mashinani pamoja na kusajili wafuasi wapya.
Viongozi hao pia waliahidi kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana, kwa lengo la kuhakikisha kaunti ya Kilifi inanufaika kimaendeleo kutoka kwa serikali kuu.

Viongozi wa Chama tawala cha UDA kaunti ya Kilifi wafanya mkutano wa kuimarisha chama mashinani
Viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya barabara nchini Aisha Jumwa, Mwenyekiti wa bodi ya hazina ya michezo, vijana na Sanaa Wakili George Kithi, Mbunge wa Ganze Kenneth Kazungu Tungule miongoni mwa viongozi wengine, ambao ni wafuasi wa chama cha UDA.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
