Mojtaba Khamenei kutangwa kiongozi mpya wa Iran

Mojtaba Khamenei kutangwa kiongozi mpya wa Iran

Iran inatarajiwa kumtangaza kiongozi mkuu mpya atakayechukua nafasi ya Ayatollah Ali Khamenei aliyeuawa wiki moja iliyopita kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel.

Mmoja wa wajumbe wa Baraza la wataalam alidokeza kwamba kuna uwezekano mkubwa mtoto wa Khamenei, Mojtaba Khamenei mwenye umri wa miaka 56, akachaguliwa kushikilia wadhifa huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi alisema viongozi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ndio watakaomchagua kiongozi wao na wala sio rais wa Marekani Donald Trump kama alivyodai.

Wakati vita vikiingia siku ya tisa, mashambulizi yalishuhudiwa kila upande.

Israel ilishambulia maghala na vituo vya kuhifadhi mafuta mjini Tehran huku Iran nayo ikivurumisha makombora na droni kuelekea Israel na katika nchi zingine za Ghuba.

Watu sita waliripotiwa kujeruhiwa huko Israel huku wanajeshi wawili wa Israel wakiuwa kusini mwa Lebanon.

Jeshi la walinzi wa mapinduzi wa Iran limesema lina uwezo wa kuendeleza mapigano hadi miezi sita na limeonya kuwa awamu inayofuata ya mashambulizi inaweza kuhusisha makombora ya kisasa ambayo hayajawahi kutumika katika vita.

Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump, alikataa kuondoa uwezekano wa kutuma wanajeshi wa ardhini nchini Iran, hatua ambayo inaweza kuongeza hatari ya vita katika eneo hilo.

Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo katika ibada ya Misa siku ya Jumapili tarehe 8 mwezi Machi, 2026 alihimiza kukomeshwa kwa vurugu na kuanzisha juhudi mpya ili kuendeleza mchakato wa mazungumzo.

Taarifa ya Mwanahabari wetu