Meli kubwa ya mizigo MV CMA CGM Cleveland yatia nanga bandarini Mombasa

Meli kubwa ya mizigo MV CMA CGM Cleveland yatia nanga bandarini Mombasa

Bandari ya Mombasa imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama lango kuu la biashara Afrika Mashariki baada ya kupokea kwa mara ya kwanza meli kubwa ya mizigo, ya MV CMA CGM Cleveland.

Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba zaidi ya makasha 6,550 na yenye urefu wa meta 300, iliwasili nchini baada ya safari kutoka Ningbo nchini China, kupitia Singapore na Colombo, Sri Lanka.

MV Cleveland ni sehemu ya huduma ya usafirishaji ya Kilima Service, inayounganisha Afrika Mashariki na masoko ya Asia na dunia kwa ujumla.

Katika bandari ya Mombasa, meli hiyo itashughulikia zaidi ya makasha 4,500, kabla ya kuelekea bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa kupokea meli hiyo, mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya Bandari nchini KPA nahodha William Ruto alisema hatua ya meli hiyo kutia nanga katika bandari ya Lamu na sasa bandari ya Mombasa ni ishara tosha ya kuongezeka kwa umuhimu wa Kenya katika biashara ya kimataifa, na kuimarisha nafasi ya bandari zake kama viungo muhimu katika sekta ya usambazaji duniani.

Taarifa ya Mwanahabari wetu.