Majani Chai aina ya Othodox yazinduliwa mnadani Mombasa

Majani Chai aina ya Othodox yazinduliwa mnadani Mombasa

Ni afueni kwa wakulima wa majani Chai baada ya Waziri wa Kilimo nchini Mutahi Kagwe kuzindua soko la mauzo ya Chai maalum ya Othodox katika mnada wa chai wa Mombasa.

Hatua hii ya serikali kuu ni ya kukuza uzalishaji na usafirishaji wa majani chai wa daraja la juu kutoka Kenya.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Mombasa, Waziri Kagwe alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu ya kuimarisha nafasi ya Kenya katika soko la majani chai ulimwenguni.

Katika mnada huo wa kwanza wa majani chai ya Othodox jumla ya kilo zaidi ya 91,000 zilizowekwa sokoni zinatarajiwa kuwaletea wakulima mapato ya juu zaidi ikilinganishwa na majani chai ya kawaida aina ya CTC.

Kagwe alidokeza kuwa serikali inafanya mazungumzo na taifa la Iran ili kufufua tena biashara ya majani Chai baina ya mataifa hayo mawili baada ya kushuka kwa usafirishaji wa majani chai mwaka jana.

Taarifa ya Pauline Mwango