Halmashauri ya bandari nchini KPA imetangaza mpango wa kuboresha huduma katika kivuko cha feri cha Likoni, unaojulikana kama “Traffic Circulation Management Plan” unaolenga kupunguza msongamano, kuongeza usalama, na kuboresha hali ya usafiri kwa zaidi ya watu laki nne na magari elfu sita, yanayotegemea kivuko hicho kila siku.
Miongoni mwa maboresho yanayotarajiwa ni pamoja na upanuzi wa maeneo ya kusubiria abiria, ujenzi wa madaraja ya watu wanaotembea kwa miguu, magati mapya ya magari, na kupanga upya kituo cha mabasi ili kuondoa vurugu na usumbufu
Pia, zaidi ya vibanda 900 vya biashara vitajengwa kwa wafanyabiashara wadogo, kuhakikisha kuwa fursa za kiuchumi zinaendelea kuwepo.
Ujenzi huo utaanza mwezi ujao upande wa Likoni na unatarajiwa kukamilika ndani ya mda wa miaka miwili.
Hatua hiyo imeungwa mkono na viongozi wa kaunti, wabunge, wafanyabiashara, na wadau mbali mbali wakisema hatua hiyo itasaidia wananchi ambao wanategemea kivuko hicho kila siku.
KPA iliahidi kuwa mradi huu utazingatia mahitaji ya watu wote wakiwemo watu wanaoishi na ulemavu na kuleta huduma salama, bora, na jumuishi.
KPA ilisema itaandaa kikao cha umma ili kuwapa wakaazi nafasi ya kutoa maoni yao kabla ya mradi huo kuanza kutekelezwa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu