Mwanaume wa umri wa makamu ahukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezeni

Mwanaume wa umri wa makamu ahukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezeni

Mahakama ya Kilifi imemhukumu kifungo cha miaka 7 gerezani mwanaume mmoja aliyepatikana na hatia kwa kesi ya biashara ya meno za ndovu baada ya uchunguzi na ushahidi kukamilika.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa alisema kuwa mshtakiwa Abdallah Mbithi ana siku 14 kisheria za  kukata rufaa endapo hajaridhishwa na hukumu hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya uamuzi wa Mahakama kubaini kwamba Mbithi alipatikana na hatia baada ya Mahakama kuzingatia ushahidi uliotolewa ikiwemo ushahidi wa mshtakiwa wa kujitetea.

Hakimu Obulutsa aidha alisema kuwa ndovu wako katika hatari kubwa ya kuuwawa hivyo basi kesi hiyo inayohusisha wanyamapori ina hukumu kali yenye kifungo cha maisha au kutoa faini ya shilingi milioni 20 hivyo mahakama imezingatia malilio yake na kumpuguzia kifungo hicho cha miaka saba.

Awali Mahakama ilielezwa kwamba mshtakiwa alipatikana na kipande cha sehemu ya ndovu iliyoshukiwa kuwa pembe ya ndovu ambapo baadaye daktari aliyefanya uchunguzi wa maabara alithibitishia mahakama kwamba kipande hicho ni sehemu ya jino la ndovu na uzani wake ni kilo 3 yenye thamani ya shilingi laki 3.

Taarifa ya Teclar Yeri.