Shirika la kutathmini ubora wa mbegu na ustawishaji wa mimea nchini (KEPHIS), limepinga vikali mswada wa marekebisho ya mbegu na aina za mimea wa mwaka 2025, uliowasilishwa katika bunge la Seneti na Seneta wa Narok, Ledama Ole Kina.
Mswada huo unapendekeza mabadiliko ya sheria ili kuruhusu muda mfupi wa kuidhinishwa kwa mbegu mpya kupitia Shirika la kutathmini ubora wa bidhaa nchini (KEBS) badala ya KEPHIS.
Mwenyekiti wa bodi ya KEPHIS, Joseph M’Eruaki, alionya kwamba ikiwa mswada huo utapitishwa kuwa sheria, unaweza kuhatarisha usalama wa wakulima, kudhoofisha viwango vya udhibiti na kufungua mianya kwa mbegu bandia na zisizofaa sokoni.
“Kama shirika la KEPHIS hatujaridhishwa na hatua ya bunge la Seneti kuhusu mswada uliyowasilishwa kwani huenda ukadhohofisha viwango vya udhibiti na kufungua miaya kwa mbegu bandia nchini, pamoja na kupoteza hadhi ya soko la bidhaa mbalimbali”, alisema Joseoh.
Mamlaka hiyo imehimiza wabunge na wadau wa sekta ya kilimo kushirikiana kwa kina kabla ya kufanya mabadiliko yoyote ya kisheria yanayogusa moja kwa moja uzalishaji wa chakula nchini.
Taarifa ya Pauline Mwango