Familia yalilia haki baada ya mtoto wao kufariki baada ya kupigwa kichwa na mwalimu

Familia yalilia haki baada ya mtoto wao kufariki baada ya kupigwa kichwa na mwalimu

Familia moja eneo la Junju kaunti ya Kilifi inalilia haki baada mtoto wao kwa jina Anestine Dzidza Tunje mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 wa Gredi ya 8 katika shule ya Msingi ya Gongoni iliyoko Junju anayedaiwa kupigwa na mwalimu hadi kuvuja damu ndani ya kichwa chake hali iliyomfanya kufariki.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya hospitali ya rufaa mjini Kilifi kaunti ya Kilifi, Alex Tunje Mzungu alisema kuwa mwanawe alianza kusema ana maumivu kwenye mwili wake hali iliyomfanya kupeleka hospitalini ili kupata huduma za matibabu katika hospitali ya Vipingo.

Mzungu alisema kuwa mwanawe alizidiwa na ndipo alipochukua hatua ya kumpeleka pia katika hospitali ya rufaa mjini Kilifi ambapo alilazwa na kisha kufariki na kulingana na ripoti ya upasuaji kutoka kwa daktari marehemu alifariki kutokana na hali ya kuvuja damu ndani ya kichwa chake.

“Nikamuuliza vipi waendeleaje akisema anaskia vibaya nikamchukua nikampeleka hospitali’’ alisema Mzungu

Kwa upande wake Jimmy Thoya na Caroline Mbeyu ambao pia ni wanafamilia waliitaka idara ya usalama kumchukulia hatua za kisheria mwalimu huyo na pia kuweka mikakati ambayo itadhibiti visa kama hivyo kutokea shuleni.

Kwa upande wake Salome Karisa ambaye ni mtetezi wa haki za watoto alikashifu kitendo hicho na kuahidi kama mashirika ya kutetea haki za kibinadamu watahakikisha haki inapatikana kwa familia hiyo.

“Tunapinga vikali kitendo kama hiki ya uvunjaji wa sheria hususan kwa haki za watoto na tunaomba yule mwalimu aliyehusika apate kuchukuliwa hatua’’ alisema Karisa

Taarifa ya Janet Mumbi