Mashindano ya kandanda ya kombe la Dola yamezinduliwa rasmi hii leo mjini Mombasa.
Mashindano hayo ambayo yanajumuisha timu ishirini kutoka kaunti za Mombasa, Kwale na Kilifi, yanatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja katika uwanja wa Mombasa Sports Club.
Akizungumza na wanahabari, Afisa wa Mawasiliano wa Kampuni ya Dola, Hassan Ibrahim, amesema mashindano haya yamelenga kuwapa vijana fursa ya kuonyesha vipaji vyao, pamoja na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kujikuza kisoka.
Aidha amebainisha kuwa mshindi wa mashindano haya atajinyakulia kitita cha shilingi nusu milioni, huku timu zitakazomaliza katika nafasi ya pili hadi ya nne zikijishindia zawadi ya kati ya shilingi laki mbili na nusu hadi elfu hamsini.
Aidha, wachezaji binafsi watakaoonyesha kiwango cha juu cha mchezo watatunukiwa shilingi elfu ishirini kila mmoja.
“Leo tunaanza ukurasa mpya wa makala ya mwaka huu kombe la SISINIDOLA Kaunti za Mombasa,kwale na Kilifi,Mshindi atapokea nusu milioni naye wa pili mpaka nafasi ya nne watanufaika na pesa hadi laki mbili wa nafasi ya nne kando na wachezaji kutuzwa.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka FKF Kaunti ya Mombasa, Allamin Abdallah, amewataka vijana wanaoshiriki kutumia nafasi hiyo kama jukwaa la kujitangaza na kujiendeleza kisoka.
“mashindano haya ni fursa kwa vijana kuonyesha uwezo walio nao kwani ukanda wa pwani inajulikana kwa mapenzi ya dhati kwa soka .”
Nao Kocha Rajab Babuu, ambaye ni msimamizi wa Mombasa Sports Club, amemtaka mfadhili wa mashindano hayo kuhakikisha kuwa wanawafuata kwa karibu wachezaji watakaoibuka na vipaji, ili kuwapa mwongozo na kuwaendeleza katika taaluma yao ya kandanda.
“Haya mashindani ni jambo zuri kwa vijana wetu na naomba mfadhili wetu wafuatilie vijana ili vipaji vyao pamoja na values ziwe katika hali shwari.”
Meshi hizo zimeongoa nanga rasmi uwanjani Mombasa Sports Club hii leo.