Business
Wafanyabiashara waomba kufunguliwa kwa soko la Matano Mane, Kaunti ya Kilifi
Wafanyabiashara katika soko la Matano Mane, eneo bunge la Vitengeni, Kaunti ya Kilifi, wameiomba serikali ya kaunti kufungua soko la eneo hilo lililojengwa miaka 15 iliyopita lakini hadi sasa halijaanza kutumika.
Wakizungumza na Coco FM, wafanyabiashara hao wamesema kuwa wanakumbwa na changamoto nyingi, hasa wakati huu wa mvua, ambapo bidhaa zao zinaharibiwa kwa kunyeshewa kutokana na ukosefu wa sehemu ya kudumu ya kufanyia biashara.
Josphat Karisa, mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, amesema kuwa wanalazimika kufanya biashara katika mazingira magumu licha ya kuwepo kwa soko lililojengwa lakini halijafunguliwa rasmi kwa matumizi.
“Tunapitia hasara kubwa wakati huu wa mvua. Bidhaa zetu zinaharibika kwa sababu hatuna mahali pa kudumu pa kufanyia biashara, ilhali kuna soko limejengwa miaka 15 iliyopita lakini halitumiki,” amesema Karisa.
Ameitaka serikali ya Kaunti ya Kilifi kuchukua hatua za haraka kuhakikisha soko hilo linafunguliwa ili wafanyabiashara waweze kuendeleza shughuli zao bila usumbufu na kujikimu kimaisha.