Sports
Arsenal Karibu Kufikia Makubaliano Mapya na Beki Gabriel
Klabu ya Arsenal ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na beki wao wa kati, Gabriel Magalhães, kuhusu mkataba mpya.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 raia wa Brazil, bado ana mkataba unaoendelea hadi mwaka 2027, lakini klabu hiyo imekuwa ikijadiliana naye kuhusu masharti mapya ya kuboresha mkataba huo.
Ikumbukwe kuwa mazungumzo hayo yamepiga hatua kubwa, na makubaliano yanaelekea kukamilika hivi karibuni.
Taarifa hiyo inakuja kama faraja kubwa kwa The Gunners wakati wanajiandaa kwa msimu wa uhamisho wa majira ya joto, ambapo wanatarajiwa kufanya usajili muhimu ili kuimarisha kikosi.
Gabriel amekuwa mchezaji wa msingi chini ya kocha Mikel Arteta, ingawa msimu wake ulimalizika mapema mwezi Aprili kufuatia majeraha ya paja yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo, beki huyo anatarajiwa kuwa fiti kabla ya msimu mpya kuanza.
Katika msimu uliomalizika wa mwaka 2024/2025, Gabriel alifunga magoli matano katika mashindano yote akiwa na Arsenal.