News
Aisha Jumwa akosolewa kutokana na matamshi yake
Jopo la ushauri la viongozi na maimamu wa Takaungu wadi ya Mnarani kaunti ya Kilifi limeeleza kusikitishwa na kauli zilizotolewa na Aisha Jumwa kuhusiana na tukio la mauaji na maziko ya kijana mmoja eneo hilo lililomtaja kama Zakariyah Kirao Charo.
Likizungumza na vyombo vya habari, jopo hilo likiongozwa na sheikh Mahadh Ali wa msikiti Maryam limemkosoa Jumwa kwa kile lilichosema ameuhujumu uislamu kutokana na kauli alizotoa kwenye mtandao wake wa kijamii wa tiktok kuhusiana na mazishi ya kijana huyo.
Sheikh Mahadh amesema Jumwa alidai kuwa familia ya marehemu haikuhusishwa ilhali walichukua wajibu wa kuihusisha familia kabla ya hatua zozote kuchukuliwa ila wanafamilia wenyewe hawakuonyesha ushirikiano akieleza kuwa jopo hilo pia liligadhabishwa na kauli za Jumwa kuhusiana na namna mchakato mzima wa mazishi ulivyofanywa.
Akiunga mkono kauli hiyo Ustadh Mohamed Khamis amesema kwenye mkao huo kuwa amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa Jumwa tangia mtafuruku huo ulipoanza akisisitiza haja ya swala hilo kutotumika kwa namna ya kuchochea wanajamii waislamu na wasio kuwa waislamu katika eneo hilo la Takaungu.

Aisha Jumwa /Picha kwa hisani
Ustadh Mohamed pia amekinzana na kauli kuwa marehemu alisilimishwa akiwa na matatizo ya kiakili akisema ni sharti swala hilo lisiingiziwe siasa.