News

Viongozi wa Kilifi Wapinga Uekezaji wa Mradi wa Kawi ya Nuklia

Published

on

Wizara ya Kawi nchini imefanya kikao cha mazungumzo na uongozi wa kaunti ya Kilifi, pamoja na wabunge na Wasimamizi wa Shirika la NUPEA kuhusu uekezaji wa mradi wa uzalishaji kawi ya Nuklia katika kijiji cha Uyombo wadi ya Matsangoni katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini katika kaunti ya Kilifi.

Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho mjini Kilifi, Waziri wa Kawi nchini Opiyo Wandayi amesema japo viongozi wa kaunti ya Kilifi pamoja na wananchi hawajaridhishwa na uekezaji wa mradi huo, mazungumzo kuhusu mradi huo bado yataendelea ili kuibuka na mwafaka kwani utasaidia pakubwa katika uzalishaji kawi.

Kwa upande wake Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro amesema msimamo wa serikali ya kaunti ya Kilifi pamoja na wananchi bado uko pale pale wa kuendelea kupinga uekezaji wa mradi huo wa mabilioni ya pesa, akisema utafiti uliofanywa umebaini kwamba mradi huo unaathari kubwa kwa wananchi.

Hata hivyo Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya amesema kama viongozi kutoka kaunti ya Kilifi hawako tayari kupokea mradi huo wa uzalishaji kawi ya Nuklia, akisema changamoto nyingi bado hazitatuliwa katika mradi huo ambazo ni athari kwa wananchi.

Kikao hicho hata hivyo kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi, Mbunge wa Kaloleni Paul Katana, Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, Mbunge wa Ganze Kenneth Tungule, Katibu katika Wizara ya masuala ya vijana na michezo nchini Fikirini Jacobs miongoni mwa viongozi wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version