Entertainment

Young Njita: Mr. Malindi ni Brand Yangu ya Biashara – Wanaonilalamikia Wanahofia Mafanikio Yangu

Published

on

Msanii wa muziki wa rap kutoka Pwani, Ramadhan Ngao Mangale maarufu kama Young Njita – Njigiri, amezungumza kwa mara ya kwanza kwa kina kuhusu mgogoro unaomkabili kuhusu jina lake maarufu – Mr. Malindi.

Akiwa mgeni kwenye kipindi cha COCO ASUBUHI wakati akizindua EP yake mpya ya nyimbo 8 iliyopewa jina “1996” (mwaka wake wa kuzaliwa), Young Njita alisisitiza kuwa jina la Mr. Malindi si tu alilolichagua kwa mapenzi, bali limekuwa sehemu ya maisha yake ya kisanii, ya biashara, na ya jamii.

“Wanaonisema hawana hoja – wana wivu tu na mafanikio yangu. Jina hilo liliibuka baada ya kushinda tuzo ndani ya mji wa Malindi, na watu wenyewe wakaanza kunitambua hivyo. Nikaamua kulitumia kujenga brand yangu,” alisema kwa kujiamini.

Kwa mujibu wa Njita, jina hilo halihusiani tu na muziki. Limekuwa kivutio katika miradi mbalimbali ya kijamii na kibiashara kama vile: Ziara kwenye vituo vya watoto yatima (orphanages), Biashara ya boti, Uzalishaji wa filamu ya Mr. Malindi na Uuzaji wa nguo za chapa ya Mr. Malindi.

“Siwezi kuwa na jina ambalo lina nguvu kiasi hiki kisha niache tu kwa sababu watu wachache wamelalamika. Kila mtu anaweza kujiita Mr. Chonyi, Mr. Kilifi, hata Mr. Coast — hakuna anayemzuia. Jina la mji si milki ya mtu mmoja,” alisisitiza Njita.

Mgogoro huu ulizidi moto baada ya Lufdon Land, kampuni inayojihusisha na matukio ya urembo kama Miss Malindi, kuandika kwenye ukurasa wao wa Facebook tarehe 12 Mei:

“Tumeona jina la Mr. Malindi likitumika na msanii tajika toka Malindi. Jina hilo linamilikiwa kihalali na kampuni ya Lufdon Land… Tumekuwa tukimpa kazi msanii huyo, lakini hatukumchagua kama Mr. Malindi Kenya. Tunaomba kwa heshima asitishe kulitumia.”

Kampuni hiyo ilieleza kuwa hawafanyi shindano la Mr. Malindi kila mwaka, na linapofanywa, hupewa mshindi mmoja pekee. Kwao, jina hilo ni brand ya heshima na sura ya kampuni, hivyo kuliona likitumika kwenye biashara nyingine kuliwafanya wachukue hatua ya kutoa onyo hadharani.

Young Njita kwa upande wake anasema hali ya watu kumtaka aachane na jina hilo si kwa sababu ya sheria, bali kwa sababu ya mafanikio yake.

“Kila mtu anapigania jina baada ya kuona nimefanikiwa nalo. Mbona miaka yote walikaa kimya? Leo hii Mr. Malindi imekuwa gumzo kwa bidii zangu wanaanza kulalamika, kivipi?”

Hili ndilo swali kuu linalozua mjadala mkali mitandaoni. Je, jina kama Mr. Malindi linaweza kuwa milki ya mtu binafsi au kampuni moja? Au linapaswa kuwa huru kwa yeyote mwenye mapenzi, asili au mchango kwa mji huo?

Kwa sasa, bado hakuna tamko la kisheria lililotolewa wazi kuhusu uhalali wa usajili huo, lakini bila shaka, huu ni mgogoro unaoibua maswali mapya kuhusu haki za wasanii, biashara za majina, na nguvu ya brand binafsi zinazojengwa na watu wa kawaida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version