News
Wauguzi kaunti ya Kilifi wasitisha mgomo
Zaidi ya wauguzi 700 kutoka kaunti ya Kilifi wamesitisha mgomo wao baada ya kufanya kikao na gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Maitha Mung’aro.
Katika kikao hicho kilichojumuisha gavana Mung’aro, naibu gavana Flora Chibule na waziri wa Afya kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo, wauguzi hao walikubali kurejea kazini baada ya gavana kuahidi kushughulikia matatizo yao.
Mung’aro alibainisha kuwa wamebuni jopo maalum litakaloangazia matatizo ya wauguzi na kuyawasilisha moja kwa moja kwa serikali ya kaunti, huku wauguzi hao wakipongeza hatua hiyo.
Miongoni mwa changamoto walizokuwa wakilalamikia ni pamoja na kupandishwa vyeo, malimbikizi ya mishahara ya wauguzi miongoni mwa changamoto zingine.
Gavana Mung’aro aliahidi kutatua matatizo yao hatua kwa hatu na kuwasihi wauguzi wote kurejea kazini.
“Tumebuni kamati ndogo ambayo itakua ikikutana na mimi kila baada ya wiki mbili ili tuangazie haya matatizo ya wauguzi tutasuluhisha polepole tuone ni vipi wauguzi wetu watafanya kazi katika mazingira mazuri, hivyo waambieni wenzenu warejee kazini kwa sababu haya matatizo yenu tutakua tunayatatua polepole”. … alisema Mung’aro.
Taarifa ya Elizabeth Mwende