News
Wauguzi kaunti ya Kilifi wasitisha mgomo

Zaidi ya wauguzi 700 kutoka kaunti ya Kilifi wamesitisha mgomo wao baada ya kufanya kikao na gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Maitha Mung’aro.
Katika kikao hicho kilichojumuisha gavana Mung’aro, naibu gavana Flora Chibule na waziri wa Afya kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo, wauguzi hao walikubali kurejea kazini baada ya gavana kuahidi kushughulikia matatizo yao.
Mung’aro alibainisha kuwa wamebuni jopo maalum litakaloangazia matatizo ya wauguzi na kuyawasilisha moja kwa moja kwa serikali ya kaunti, huku wauguzi hao wakipongeza hatua hiyo.
Miongoni mwa changamoto walizokuwa wakilalamikia ni pamoja na kupandishwa vyeo, malimbikizi ya mishahara ya wauguzi miongoni mwa changamoto zingine.
Gavana Mung’aro aliahidi kutatua matatizo yao hatua kwa hatu na kuwasihi wauguzi wote kurejea kazini.
“Tumebuni kamati ndogo ambayo itakua ikikutana na mimi kila baada ya wiki mbili ili tuangazie haya matatizo ya wauguzi tutasuluhisha polepole tuone ni vipi wauguzi wetu watafanya kazi katika mazingira mazuri, hivyo waambieni wenzenu warejee kazini kwa sababu haya matatizo yenu tutakua tunayatatua polepole”. … alisema Mung’aro.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Kongamano la kukomesha visa vya dhuluma za kijinsia Taita Taveta

Idara ya usalama kaunti ya Taita taveta imeandaa kongamano maalum ili kujadili namna ya kukomesha visa vya dhuluma za kijinsia na kingono kaunti hiyo.
Kongamano hilo limefanyika katika eneo la Werugha, eneo bunge la Wundanyi kaunti ya Taita Taveta na limejumuisha maafisa wakuu wa serikali ya kaunti hiyo, viongozi wa kijamii pamoja na wananchi.
Kamishna wa kaunti ya Taita Taveta Josephine Onunga alibainisha kuwa kuna ongezeko la visa 186 ndani ya miaka miwili, eneo bunge la Taveta likirekodi visa 64 huku Wundanyi ikirekodi 38 hivyo kuwataka wakaazi kushirikiana na idara mbalimbali za usalama ili kukomesha visa hivyo.
“Tunapendekeza ushirikiano mkubwa zaidi na zaidi kuanzia mashinani kila boma tulindane, tujuliane hali, hakikisha unamlinda mwenzako”, alisema Onunga.
Kwa upande wao Wanaharakati wa kupambana na dhuluma za kijinsia wakiongozwa na Mary Mgola walieleza hofu yao kutokana na ongezeko la visa hivyo hasa maeneo ya mashinani.
Walisema ukosefu wa mashahidi wa kutosha wakati kesi hizo zinapowasilishwa Mahakamani, ikitajwa kama changamoto kuu wakati wa kusuluhisha kesi hizo.
Mgola aliitaka Mahakama kuhakikisha wanatoa ulinzi wa kutosha kwa mashahidi wa kesi za dhuluma za kijinsia na kingono.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
JSC, yashutumu mashambulizi dhidi ya Idara ya Mahakama

Tume ya huduma za Mahakama nchini JSC imeshtumu vikali tabia inayoendelea kusheheni nchini ya kuwashambulia hadharani majaji kuhusu uamuzi wanaoutoa wa dhamana kwa washukiwa wa kesi za maandamano.
Katika taarifa iliyotolewa na JSC kupitia Katibu wa Idara wa Tume hiyo Winfridah Mokaya, ilisema tume hiyo imeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu athari za maamuzi ya hivi majuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Nanyuki.
Katika Mahakama hiyo zaidi ya watu 100 waliokamatwa kutokana na maandamano ya Julai 7 katika kaunti ya Laikipia waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 50 pesa taslimu kila mmoja baada ya kushtakiwa kwa uharibifu wa mali.
“Tunashangazwa na tabia ya kuwashambulia majaji hadhara kuhusu uamuzi wanaotoa kuhusu washukiwa wa maandamano ya Juni 25 na Julai 7 wakati wa maandamano ya Sabasaba na Mahakama iko kisheria na inafuata sheria”, alisema Mokaya.
Winfridah ambaye pia ni Msajili mkuu wa Idara ya Mahakama nchini amesema wakosoaji akiwema Jaji mkuu wa zamani David Maraga ambao wanashinikiza kuondolewa kwa mashtaka ya ugaidi dhidi ya waandamanaji, akisema wanafaa kuheshimu mahakama.
Wakati huo huo ameonya kwamba mashambulizi dhidi ya idara ya Mahakama huenda yakasambaratisha shughuli za kupatikana haki kwa wananchi.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi