Business
Wafanyabiashara Wakosoa KRA Kuhusu Ushuru wa Juu na Huduma Duni
Baadhi ya wafanyibiashara mjini Malindi kaunti ya Kilifi wanalalamikia kupanda kwa gharama ya maisha sawa na ushuru wa biashara wakati mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini, KRA ikitangaza ongezeko la ukusanyaji wa ushuru kwa asilimia 6.8 katika mwaka wa kifedha 2024/2025.
Wakiongozwa na Kenza Ondiek wafanyibiashara hao wanasema kuwa ongezeko la ushuru nchini limeathiri pakubwa ustawi wa biashara huku uboreshaji wa miundomsingi ukiwa katika viwango vya chini.
Ondiek ameiomba serikali kuhakikisha kuwa inaboresha maisha ya wananchi kupitia mapato ya ushuru hasa baada ya mamlaka ya KRA kukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.61 katika mwaka wa kifedha 2024/2025 ikilinganishwa na trilioni 2.40 za mwaka kifedha 2023/2024.
Ondiek aidha ameiomba serikali kuwajibikia kikamilifu matumizi bora ya fedha za ushuru zinazokusanywa nchini ili kubadilisha maisha ya wananchi badala ya kuangazia njia za kuongeza kiwango cha makato ya ushuru pekee kwa wananchi.
Haya yanajiri huku mamlaka ya KRA pia ikifichua kupitisha makadirio yake ya ukusanyaji wa ushuru kutoka kwa shilingi trilioni 2.56 hadi shilingi trilioni 2.61 kwa mwaka wa kifedha 2024/2025.