Entertainment

#UlijanjarukaVipi! Safari ya Mpishi Nguli, Don Moses: Kutoka Kukosa Karo Hadi Kuwa Head Chef

Published

on

Katika dunia ya leo ambapo changamoto za kiuchumi zimewaacha vijana wengi wakihangaika, simulizi ya Don Moses ni mwanga wa matumaini kwa wengi.

Akiwa mgeni katika kipindi cha Janjaruka 254, kinachorushwa kila siku ya wiki kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, Moses alisimulia safari yake ya ajabu kutoka kwa kijana aliyezuiwa na karo ya shule hadi kuwa mpishi mashuhuri hadi kuwa Head Chef aliyesimamia wapishi waliosomea fani hiyo chuoni.

Baada ya kuhitimu kidato cha nne, Moses alikuwa ameweka ndoto ya kujiunga na chuo lakini maisha yalikuwa na mpango tofauti. Mama yake alipata ajali mbaya, hali iliyolazimu familia kuhamishia raslimali kwenye matibabu badala ya karo yake ya chuo.

“Nilijua wazi kuwa singeweza kulazimisha familia ichague kati ya maisha ya mama na elimu yangu. Ilibidi nitafute njia mbadala,” anasema Moses.

Jiko la YouTube: Darasa la Ukombozi

Akiwa hana karo, lakini akiwa na shauku, Moses alianza kujifunza sanaa ya upishi kupitia video za YouTube. Binamu yake, Moses Gambo, ndiye aliyemfungulia mlango wa maarifa kwa kumtambulisha kwenye tutorials mbalimbali mtandaoni.

Ni ujuzi huo wa mtandaoni uliomfungulia milango ya ajira katika hoteli za kifahari, ambapo aliweza kupanda ngazi hadi kuwa mpishi mkuu (Head Chef) — akiongoza wapishi waliopitia vyuo vya kitaaluma. Ni mafanikio ambayo wengi hawakuyatarajia kutoka kwa kijana ambaye hakuingia darasa la kawaida, bali alikaa mbele ya skrini.

“Najua kwenye upishi kuna kupika mashendea ama kupika chakula kibaya ila sijawahi kufeli. Siku zote mimi ni makini na ratio ya viungo. Ndiyo silaha yangu,” anasema kwa kujiamini.

Mwaka wa Mageuzi: 2020

Kama ilivyokuwa kwa wengi, mwaka wa janga la COVID-19 – 2020 – ndiyo ulikuwa mwaka wa mabadiliko makubwa kwa Moses. Akiwa na muda mwingi na motisha mpya, alianza kupika kibiashara, akihudumia watu waliokuwa majumbani.

“Kabula ya hapo, nilikuwa napika kwa kujifurahisha tu. Lakini corona ilinifungua macho. Nikaanza kuona kuwa mapishi ni biashara yenye nguvu,” anasema Moses.

Karo Iliyogeuka Mtaji

Kipindi fulani baadaye, Moses alipata nafasi ya kujiunga na chuo hatimaye. Lakini kwa mshangao wa wengi, alikataa ofa hiyo kwa hiari na kuomba fedha hizo zitumike kupanua biashara yake ya upishi.

“Nitamudu gharama ya chuo siku moja. Kwa sasa, najenga misingi. Muda wa kusoma utafika,” anasema.

💡 Ushauri kwa Vijana: Anza na Kile Kilicho Mkono Wako

Don Moses sasa ni sauti ya matumaini kwa vijana wengi wanaohisi kuwa elimu ya juu au mtaji mkubwa ndio tiketi pekee ya mafanikio. Anasisitiza umuhimu wa kuanza na huduma, si lazima mtaji.

“Kama huna kazi wala mtaji, toa huduma kwanza. Ukiwa na bidii na ubunifu, malipo yatafuata,” anashauri.

Leo hii, sehemu kubwa ya mapato ya Moses huingia moja kwa moja kwenye ununuzi wa vifaa bora vya upishi, huku akiendeleza ndoto yake ya kuwa mmoja wa wapishi wakubwa zaidi nchini Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version