News
Propaganda zahujumu zoezi la utoaji chanjo Kilifi
Viongozi wa kijamii katika kaunti ya Kilifi wameeleza kuwa watoto wengi wanakosa kupata chanjo kufuatia dhana potovu zinazoenezwa miongoni mwa wanajamii.
Wakiongozwa na Mumina Halaso, viongozi hao wa kijamii walisema kuwa dhana potovu huchukua nafasi kubwa kwa sababu wanajamii hukosa hamasa za kutosha kabla ya mazoezi ya chanjo kutekelezwa.
Halaso alisema kuwa viongozi wa kijamii wana nafasi nzuri kupitia idara ya afya kitengo cha afya ya nyanjani kuwaelimisha wanajamii kuhusiana na maswala mbalimbali ya afya.
Akitolea mfano wa zoezi la utoaji wa chanjo za rubella na homa ya matumbo, Halaso alisema kuwa idadi kubwa ya wazazi walisusia kuwapa wanao chanjo hizo kutokana na wingi wa propaganda kuhusu chanjo hizo.
“Kuna umuhimu wa wadau mbalimbali kutumika katika kutoa hizi hamasa kuhusiana na umuhimu wa chanjo” Ameongeza Halaso.
Alikariri haja ya maafisa wa afya ya nyanjani pia kufuatilia kwa kina watoto walioanza chanjo na kukosa kuendeleza.
Taarifa ya Hamis Kombe