News
Kindiki: Serikali kuu itaimarisha uchumi wa taifa
Naibu wa Rais Prof. Kithure Kindiki amesema serikali kuu inaendeleza mikakati ya kuimarisha taifa hili kiuchumi.
Akiwahutubia wakaazi wa Garsen kaunti ya Tana River, Prof. Kindiki alisema ni jukumu la serikali kuu kuwawezesha Wakenya na makundi ya kibiashara kifedha kupitia mpango wa Bottom Up, ili taifa la Kenya liimarike kupitia mikakati ambayo imewekwa na kuafikia malengo hayo.
Prof. Kindiki pia alisema ikiwa Wakenya watawezeshwa kifedha ili kuanzisha biashara mbalimbali taifa la Kenya litaanza kuimarika kiuchumi.
Vilevile, Prof. Kindiki aliwakosoa baadhi ya wanasiasa ambao huwakumbuka wananchi wakati wa uchaguzi kwa kuwapa fedha na bidhaa zingine ili kuwarai wapigiwe kura na kusema ni jukumu la viongozi kuwawezesha wananchi kupitia miradi ambayo itawafaidi maishani kwani ni haki yao kikatiba.
Prof. Kindiki, pia aliwashinikiza wenyeji na viongozi wa kaunti ya Tana River na kanda ya pwani kwa jumla kushirikiana na serikali kuu ipasavyo na pia kuchagua rais Ruto mwaka wa 2027, ili aendelee kuiboresha nchi hii.
Taarifa ya Janet Mumbi