Wakfu wa George Kithi kwa mara nyengine umepata Tuzo za Africa Champions Awards kwa kutambulika kama Shirika linalotegemewa na wengi katika jamii.
Tuzo hizo za Africa Champions Awards ambazo ni Tuzo za kimataifa zilifanyika katika hoteli moja kaunti Mombasa zikilenga kuwapa motisha wadau mbalimbali, mashirika, Wanahabri pamoja na wawekezaji.
Masuala yaliyoangaziwa zaidi na wasimamizi wa Tuzo hizo na ambayo yalichangia Wakfu wa George Kithi kupata Tuzo hizo ni pamoja na juhuzi zinazoendeleza na Wakfu huo za kuiwezesha jamii ya kaunti ya Kilifi kujiimarisha zaidi katika masuala mbalimbali.
Mpango wa hivi majuzi wa kuwasaidia zaidi ya wakaazi 5,000 kutoka kaunti za Pwani kwa matibabu ya bure kwenye kambi ya matibabu ya bila malipo iliyoandaliwa katika uwanja wa chuo kikuu cha Pwani pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wasiojiweza, ni kati ya vigezo vilivyoangaliwa na wasimamizi wa Tuzo hizo za Africa Champions Awards.
Wakfu huo pia ulitambulika kwa juhudi zake za kuendelea kuisaidia jamii kujiimarisha kiuchumi kama dhamira ya Mkurugenzi wa Wakfu huo Wakili George Kithi, huku suala la kukuza vipaji na kufungua milango ya mustakabali ulio bora zaidi kwa jamii ukichangia zaidi Wakfu huo kupata Tuzo hizo.
Hata hivyo Wakili George Kithi, alipongeza Waandalizi wa Tuzo hizo za Africa Champions Awards kwa kutambua juhudi zinazoendelezwa na Wakfu wa George Kithi pamoja na mipango na mikakati ya Wakili huyo kwa jamii ya kaunti ya Kilifi.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
