Rais Ruto: Sina mipango ya kuongeza miaka ya uongozi

Rais Ruto: Sina mipango ya kuongeza miaka ya uongozi

Rais William Ruto amevunja kimya chake kuhusu hatamu ya uongozi na kuwakosoa wale wanaoshinikiza kuendelea kusalia madarakani kwa miaka 20 licha ya Katiba ya Kenya kuweka wazi kwamba hatamu ya rais ni mihula miwili.

Rais Ruto aliwataka viongozi kuondoa fikra hizo na kuangazia maendeleo, akisema wadhfa wa urais sio kitu rahisi vile baadhi ya viongozi wanavyofikiria na kwamba wadhfa huo una changamoto nyingi.

Akizungumza jijini Nairobi, Rais Ruto alisema mda wake wa uongozi ni mihula miwili na utakapokamilika basi ataondoka madarakani na kumuachia kiongozi wengine atakayechaguliwa na wakenya kuwa rais kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi.

“Kuna watu wengine wako na tabia mbaya, wakaenda wakasema huyu mtu amesema atakuwa rais miaka ishirini kwani watu wanafikiria hii kazi ya rais ni kazi rahisi ya kupigiwa kelele kila siku, mimi nangojea siku nitatoka hapa niende mwengine achukue asonge ama namna gani”, alisema rais Ruto.

Kauli yake ilijiri baada ya viongozi mbalimbali nchini hasa wale wanaoegemea upande wa serikali wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei, wakipendekeza kubadilisha baadhi ya vipengele vya Katiba ili kuruhusu hatamu ya uongozi kurefushwa hadi miaka 7 badala ya miaka 5 kwa mujibu wa Katiba ya Kenya.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi