Katibu katika Wizara ya Elimu nchini Julius Bitok, amesisitiza kwamba elimu ya shule za msingi na zile za upili nchini ingali bila malipo na kwamba mpango huo utaendelea.
Bitok, alipinga vikali tetesi ambazo zinaendelezwa nchini kwamba serikali inapanga kusitisha ufadhili wa masomo, akisema mpango wa elimu ya bila malipo utaendelea kote nchini hasa katika shule za umma.
Bitok alisema Wizara ya elimu nchini kwa ushirikiano na hazina ya kitaifa itaendelea kutoa fedha kwa shule ili kuhakisha sekta ya elimu inaboreshwa zaidi kote nchini.
“Hakuna mipango yoyote ya kusitisha ufadhili wa masomo, bado utaendelea kwa kuhakikisha shule za msingi na upili ni bure na tunashirikiana na hazina ya kitaifa ili kuhakikisha ufadhili wa elimu unatekelezwa”, alisema Bitok.
Wakati huo huo alisema serikali imepanga kwamba matokeo ya mtihani wa kitaifa wa gredi ya tisa KJSEA yatatangazwa tarehe 11 mwezi Disemba na wanafunzi kupangiwa shule baada ya matokeo hayo sawa na barua za shule walizoitwa kutolewa kabla ya sherehe za Krismas.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
