Kamati ya kitaifa kuhusu tuzo za Jamhuri imempongeza Wakili George Kithi kwa kutambuliwa kama shujaa wa afya, haki na masuala yanayoathiri jamii kwenye tuzo za kitaifa za mwaka 2025.
Utambuzi huu wa kifahari unasherehekea kujitolea kwake katika kupigania haki, maendeleo ya afya, na uongozi wa jamii unaoleta mabadiliko.
Kamati hiyo ilimtaja Kithi kama mwanasheria aliyebobea katika utumishi wa umma na mwenye huruma, na ambaye ameonyesha mara kwa mara kwamba uongozi hauhusu cheo, bali madhumuni na huduma zinazofaidi jamii.
Imetaja juhudi za wakili huyo katika kuboresha upatikanaji wa hudumu bora za afya, kusaidia programu za matibabu za kijamii, na kuwawezesha wanawake na vijana katika kaunti ya Kilifi kama zinazogusa maisha mengi.

Wakili George Kithi akisaidia mgonjwa aliyefika kusaka matibabu wakati wa kambi ya wiki ya matibabu ya bila malipo katika chuo kikuu cha pwani mjini Kilifi.
Kupitia wakfu wa George Kithi Foundation, kamati hiyo ilidokeza kuwa matumaini ya wengi na ndoto zilizohamasishwa vimerejeshwa na kukuza kizazi kipya cha wakazi wanaoendeshwa na malengo.
Katika sekta ya sheria, Kithi ametajwa kusimama kidete kwa usawa, ukweli, na uwajibikaji, sifa zinazoendelea kutia imani katika maono yake ya kuweko na Kilifi bora na jumuishi zaidi.

Wakili George Kithi akitangamana na baadhi ya wakaazi kwenye kambi ya wiki ya matibabu ya bila malipo katika chuo kikuu cha pwani mjini Kilifi.
Wamesifia utendakazi wake kama unaoziba pengo kati ya sheria, uongozi na ubinadamu unaoendelea kuunda safari yake na kuwatia moyo wengi kote nchini.
“Tuzo hii ya mwaka 2025 inasimama kama utambuzi wa kitaifa wa ujasiri wako, huruma, na kujitolea kwa mabadiliko ya umma”. imesema taarifa ya kamati hiyo.
Taarifa ya Joseph Jira
