Maafisa wa upelelezi eneo la Nyali, kaunti ya Mombasa, wamemkamata mwanamke anayedaiwa kupanga njama ya wizi dhidi ya mpenzi wake raia wa uingereza baada ya kumwalika nyumbani kwake.
Mshukiwa huyo, Samira Mumbi Kiarie almaarufu Samira, anadaiwa kumlaghai mwingereza huyo kwa miezi kadhaa mtandaoni kabla ya kupanga njama ya kumvutia katika nyumba yake eneo la Nyali.
Kwa mujibu wa maafisa wa DCI, dakika chache baada ya mwanaume huyo kuingia ndani, wanaume wawili walivamia nyumba hiyo mmoja akijitambulisha kama mume wa Samira na mwingine kama afisa wa polisi.
Inasemekama walimtishia raia huyo na kumlazimisha kuhamisha zaidi ya shilingi laki nane kupitia simu kabla ya kutoweka.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa kina wa kijasusi, maafisa wa DCI walifanikiwa kumtia mbaroni Samira pamoja na mshirika wake Paul Webster Mangeni, maarufu Paulo.
Ilibainika kuwa wawili hao ni sehemu ya genge linalowalenga wageni kupitia mitandao ya kijamii na kuwaibia.
Watuhumiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nyali wakisubiri kufikishwa mahakamani huku msako ukiendelea kumtafuta mshukiwa mwingine aliyetoroka.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
