Shehena ya sigara haramu yanaswa bandarini Mombasa

Shehena ya sigara haramu yanaswa bandarini Mombasa

Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA) kwa ushirikiano idara ya usalama imekamata shehena ya sigara haramu milioni 9.5 katika bandari ya Mombasa zilizokuwa zimefichwa ndani ya vifurushi vya sodo.

Naibu Kamishna wa KRA anayesimamia udhibiti wa mipaka Chege Macharia, alisema sigara hizo za thamani ya shilingi milioni 200 zilikuwa zimetoka Thailand kupitia meli ya CMA CGM, ilitangazwa kimakosa kuwa maboksi 1,100 ya sodo.

Macharia alisema kufuatia ushirikiano wa kimataifa na taarifa kutoka Idara ya Forodha ya Marekani, waligundua kwamba shehena hiyo haikuwa na sodo bali sigara haramu aina ya Supermatch zenye nembo ya Mamlaka ya ushuru ya Uganda (URA) na maandishi ya “For export.”

“Tumefanikiwa kunasa shehena ya sigara haramu milioni 9.5 ambazo zilikuwa zimefichwa kwenye maboksi ya Sodo baada ya kupata taarifa kutoka kwa makala wa forodha na hizi sigara ni hatari kwa maisha ya binadamu na hata pia kwa mapato ya serikali”, alisema Macharia.

Macharia alisema hatua hiyo inaonyesha mafanikio makubwa katika vita dhidi ya bidhaa za magendo na ukwepaji wa ushuru, akiongeza kwamba biashara hiyo haramu inaathiri mapato ya serikali na afya ya wananchi.

Taarifa ya Mwanahabari wetu