Serikali ya kaunti ya Mombasa imeshinikizwa kuheshimiana na bunge la Kaunti hiyo katika utendakazi wao, kwani malumbano kati yao yanaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo mashinani.
Akizungumza na wandishi wa habari, seneta wa Mombasa, Mohammed Faki, alisema kuwa bunge la kaunti linatambulika kikatiba kupitia sheria ya ugatuzi, hivyo kulikandamiza ni kukosa kuliheshimu kama taasisi muhimu ya utawala.
Hata hivyo, aliwataka wawakilishi wa wadi kushirikiana na serikali ya kaunti ili kuhakikisha maswala muhimu waliyowaahidi wananchi yanatekelezwa ipasavyo.
Wakati huo huo Faki alisema kuna masuala mengi yanayostahili kujadiliwa ndani ya bunge hilo, ikiwemo uimarishaji wa miundombinu ya barabara, kupitishwa kwa mawaziri walioteuliwa pamoja na mambo mengine muhimu yanayohusu ustawi wa wananchi wa Mombasa.
Kauli hiyo ilijiri siku chache baada ya kushuhudiwa vurugu wakati wa kikao kati ya kamati ya ardhi ya bunge la kaunti na mafisa wa idara hiyo wakiongozwa na waziri Mohamed Hussein.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
