National News
Muturi Atemwa Katika Baraza la Mawaziri
Rais William Ruto amefanya mabadiliko kadhaa katika baraza lake la mawaziri na kuwateua watu wengine kushikilia nyadhfa hizo huku aliyekuwa Waziri wa utumishi wa umma nchini Justin Muturi akitemwa nje.
Katika chapisho rasmi la gazeti la serikali ambalo limetiwa saini na mkuu wa utumishi wa umma nchini Felix Koskei, Rais Ruto kwa kuzingatia kipengele cha 152 ibara ya 2 ya katiba, amemteua Hanna Wendot Cheptumo kushikilia Wizara ya Jinsia, utamaduni na turathi.
Mwengine ni Mbunge wa Mbeere Geoffrey Kiringa Ruku ambaye ameteuliwa kushikilia Wizara ya utumishi wa umma nchini, Wizara ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Justin Muturi ambaye ametemwa nje ya baraza la mawaziri.
Kiongozi wa taifa, ametumia mamlaka yake ya kikatiba kwa kuzingatia kipengele cha 152 ibara ya 5{a}, na kufanya uhamisho wa mawaziri kutoka Wizara moja hadi nyingine ambapo Waziri wa mazigira na misitu nchini Adan Duale amehamishiwa Wizara ya Afya nchini huku Deborah Barasa ambaye alikuwa akishinikilia Wizara hiyo akihamishiwa Wizara ya Mazingira na misitu.
Uteuzi huo mpya wa mawaziri pamoja na uhamisho, umejiri siku moja tu baada ya Rais Ruto kufanya kikao na viongozi kutoka mlima Kenya pamoja na viongozi wengine kutoka maeneo ya Magharibi mwa Kenya sawa na kikao tofauti na Viongozi wa kidini.