Sports
Uingereza yawapa wapinzani onyo baada ya kuichapa Serbia 5-0, Haaland apiga mabao matano kwa Norway
Timu ya taifa la Uingereza ilituma onyo kali kwa wapinzani wao wa Kombe la Dunia baada ya kuifumua Serbia 5-0 katika mchezo wa kufuzu siku ya Jumanne, huku Erling Haaland akifunga mabao matano na kuisaidia Norway kuendeleza rekodi ya ushindi wa asilimia 100.
Kwingineko barani Ulaya, Ureno na Ufaransa ziligeuza matokeo baada ya kuwa nyuma na kupata ushindi wa pili mfululizo katika harakati zao za kufuzu kwa michuano ya mwakani itakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Ubora wa kikosi cha Thomas Tuchel ulitiwa shaka baada ya ushindi hafifu wa 2-0 dhidi ya Andorra siku ya Jumamosi huko Villa Park, lakini safari hii walitoa jibu tosha.
Uingereza ilidhibiti dakika za mwanzo mjini Belgrade na kufungua ubao dakika ya 33, wakati Harry Kane alipofunga bao lake la 74 la kimataifa kwa kichwa akimalizia kona ya Declan Rice. Wageni waliongeza bao dakika mbili baadaye, Noni Madueke akimalizia pasi nzuri ya kichwa kutoka Morgan Rogers na kumchambua kipa wa Serbia, Djordje Petrovic.
Bao la tatu lilipatikana dakika ya 52, Ezri Konsa akipiga shuti kufuatia mpira uliorudi baada ya adhabu ndogo na kufunga bao lake la kwanza la kimataifa.
Mpira mwingine wa adhabu uliopigwa na Rice ulipelekea bao la nne, Marc Guehi akiteleza na kufunga kufuatia faulo iliyofanywa dhidi ya Kane na Nikola Milenkovic, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja.
Mbadala Marcus Rashford alifunga kwa mkwaju wa penalti mwishoni na kukamilisha usiku bora kwa Uingereza.
Uingereza sasa inaweza kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya nane mfululizo kwenye mchezo wao ujao wa Kundi K dhidi ya Latvia mwezi ujao.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Albania ilipanda hadi nafasi ya pili baada ya kuishinda Latvia 1-0 jijini Tirana.