News
Murkomen: Machifu Walio Maeneo Hatari Kupewa Bunduki
Waziri wa usalama ndani Kipchumba Murkomen ameamrisha machifu ambao wanahofia maisha yao kutoka kaunti tano ambazo zinashuhudia msukosuko wa kiusalama kupewa bunduki kujihami.
Waziri Murkomen amesema machifu hao kutoka kaunti za Meru, Isiolo, Marsabit, Laikipia na Samburu, watasajiliwa pamoja na kupewa mafunzo ya kumiliki silaha kabla ya kupewa bunduki na serikali kama njia moja wapo ya kulinda usalama wao wanapokuwa kazini.
Akizungumza katika kikao cha kiusalama, Murkomen amesema Wizara ya usalama amepokea malalamishi kutoka kwa machifu ambao wamesema wanawafahamu wezi wa mifugo na majangali wengine ila wanahofia kuwakamata kutokana na uoga wa kuvamiwa.
Kauli yake imejiri baada ya Machifu ambao wanaishi katika maeneo yanayoshuhudiwa utovu wa usalama kulalamikia kwamba maisha yao yako hatarini.