News
Murkomen Amshambulia Muturi kwa Kushikilia Nyaraka za Siri za Serikali
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amemkashifu aliyekuwa Waziri la utumishi wa umma Justin Muturi kwa madai ya kushikilia nyaraka muhimu za siri za serikali
Waziri Murkomen amesema hatua kama hiyo inaweza kuchangia athari za kisheria.
Akizungumza na Wanahabari, Waziri Murkomen ameeleza kwamba Muturi alipokuwa Mwanasheria mkuu nchini aliapa kutunza siri alipokuwa akishughulikia stakabadhi za serikali na kudai kushangazwa na Muturi.
Waziri Murkomen amedai kwamba anashuku Muturi ana nia mbaya ya kunyima stakabadhi za serikali, akidai kwamba katika mataifa mengine mtu kama huyo angeweza kufungwa jela.
Waziri huyo pia alirejelea kesi ya 2016 iliyomhusisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ambaye alishtakiwa kwa kutumia barua pepe ya kibinafsi kushughulikia maswala yanayohusiana na kazi, ambapo alitishia usalama wa taifa.
Murkomen hata hivyo imeitaka idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI, ile ya ujasusi nchini NIS pamoja na Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini ODPP kumkamata Muturi na kumfungulia mashtaka.
Itakumbukwa kwamba Muturi alitimuliwa kazini na Rais William Ruto kutokana na msimamo wake wa kuikosoa serikali kufuatia visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela, ufisadi ndani ya serikali pamoja na kudhalilishwa kwa mawaziri nchini.