News
Polisi wawili wafariki kwa kupigwa shoti ya umeme
Maafisa wawili wa polisi wamefariki baada ya kunaswa na umema kwenye kituo cha polisi cha Ainamoi eneo bunge la Ainamoi kaunti ya Kericho wakati walipokuwa wakijaribu kuweka nguzo ya mawimbi ya redio katika kituo hicho.
Tukio hilo lilitokea wakati maafisa hao wawili—mmoja wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) na mwingine wa jeshi la polisi—waliposhindwa na uzito wa mlingoti, ambao ulianguka na kugusana na nyaya za umeme za moja kwa moja kutoka kwenye njia ya umeme iliyokuwa karibu.
Kulingana na afisa wa utawala wa eneo hilo, kisa hicho kilitokea bila kutarajiwa, na maafisa wote wawili walikufa papo hapo kutokana na shoti ya umeme.
Msamaria mwema aliyekuwa akiwasaidia maafisa hao alipata majeraha madogo baada ya kuangushwa chini na mshtuko mdogo.
Kwa sasa amelazwa katika kituo cha afya cha Ainamoi na inasemekana hali yake inaendelea vyema.
Miili ya maafisa hao wawili ilitolewa katika eneo la tukio na inakisiwa kuwa ilipelekwa katika makafani ya Lazaro katika Hospitali ya Siloam mjini Kericho.
Taarifa ya Joseph Jira