News
KNCHR yatoa idadi ya waliofariki kwenye maandamano
Tume ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu nchini KNCHR imesema watu 8 wamethibitishwa kuaga dunia wakati wa maandamano yaliofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Tume hiyo ilisema watu hao walifariki baada ya kupigwa risasi na maafisa wa polisi katika maandamano ya kuwaenzi vijana wa Gen Z waliofariki wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka wa 2024, mwezi Juni 25, mwaka jana 2024.
KNCHR ilisema watu hao waliofariki ni kutoka kaunti 6 tofauti ambapo watu 2 kutoka kaunti ya Machakos, wawili kaunti ya Makueni, mmoja kaunti ya Nakuru, mmoja kaunti ya Kiambu, mmoja kaunti Uasin Gishu na mwengine katika kaunti ya Nyandarua.
Tume hiyo pia ilidokeza kwamba watu 400 walijeruhiwa katika maandamano hayo miongoni mwao ikiwa ni wanahabari, waandamanaji na maafisa wa polisi huku ikisema wengi wao ni wale waliokuwa wanahitaji matibabu ya dharura.
Hata hivyo tume hiyo iliweka wazi kwamba kuna baadhi ya watu ambao walikamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi, na hawapo katika vituo vya polisi huku ikikashifu vikali hatua ya mamlaka ya mawasiliano nchini CA, kwa kuzima mawimbi ya vituo vya habari nchini.
Taarifa ya Joseph Jira